Sunday, July 24, 2022

MFUNGWA WA FIKRA


Moja ya sababu kubwa ambayo inalifanya bara la Afrika kuendelea kuwa kwenye kiwango kikubwa cha umasikini ni ufungwa wa fikra kwa viongozi wengi hali ambayo imekuwa ni donda ndugu kwa vizazi na vizazi.
Miaka zaidi ya hamsini Tangu Afrika ilipoanza kupata uhuru wa bendera hata sasa bado nchi nyingi zipo kwenye gereza la fikra, kuanzia watawala mpaka watawaliwa. Tumeshindwa kujitegemea kwa asilimia walau 75 hivi kila kitu tunategemea watu kutoka Amerika ya kaskazini, Ulaya na hata baadhi ya nchi za Asia kufanya maamzi ya namna ya kuendesha nchi zetu...
Miaka zaidi ya hamsini ya uhuru wa bendera kwa Mwafrika, hana uwezo wa kufanya maamzi yanayojitegemea, miaka zaidi ya hamsini nchi nyingi hazina hata kiwanda kimoja cha dawa muhimu za binadamu, pamoja na wingi wa madini ya aina mbalimbali katika ardhi ya Afrika lakini bado tunaagiza kuanzia vyeni mpaka magari kwenye mabara ambayo malighafi wanachukulia Afrika.

Hali hiyo imefanya hata mifumo ya uendeshaji wa mambo mengi muhimu kuwa katika hali ya utegemezi, elimu yetu ikiwa kwenye muundo ambao unamfanya mtu anapohitimu tageti ya kwanza ni kuajiriwa sio kuwa na fikra zenye lengo la kuongeza fursa za ajira, elimu yetu haitupi mwanga wakuliona bara letu kama fursa inayojitgemea na kila mmoja anaweza kuitumia na kumpatia uwanda mpana wa kulivua vazi la umasikini linalotesa familia nyingi hapa kwetu Afrika.

Ufungwa wa fikra ni mbaya kuliko ufungwa wa kuwa gerezani, akili inaposhindwa kufanya kazi sawasawa hulazimika kuwa tegemezi, maana akili tegemezi huwa haina uwezo wa kuziona fursa na hata ikiziona fursa huwa inalazimika kuhitaji msaada wa ziada ili kuweza kuzitumia.
Hili ndiyo koti ambalo limeshindwa kutuachia kwa muda mrefu kuanzia vizazi vya uhuru mpaka kizazi cha connection (dot.com generation) ambapo bado hatuamini katika kujitegemea na kusimama wenyewe...

Kila nikiwatazama vijana wenzangu tukiwa katika vijiwe mbalimbali, namna tunavyoishi kwa matumaini na matarajio ya kupokea muujiza Fulani, nashindwa kuwalaumu kwa sababu nikirudi nyuma kuanzia kwenye familia zetu, wazazi nao wanaishi kwa matumaini, kutwa wakipiga simu wakiulizia nafasi za kazi kwenye mashirika na serikalini, nina kijana wangu amemaliza chuo na amefaulu vyema sana hakuna nafasi hapo kwenu hata umshike mkono....
Nikikaa chini tena nahisi kuwalaumu wazazi kwa nini umemsomesha mtoto, amekuwa na elimu ya juu kuliko hata wewe bado unahangaika kumtafutia connection kwa nini usimwache ajitegemee, ndipo nakumbuka elimu ya kujitegemea ilikwenda na Julius Kambarage Nyerere katika kaburi lake pale Buatima, ahaa sasa tuna elimu ya faulu vizuri upate kazi nzuri, faulu vizuri maana mjomba wako yupo kwenye idara Fulani atakuvusha na wewe utakuwa na kazi nzuri...

Kijana tangu akiwa shule ya msingi anawaza kuajiriwa, anawaza kuna mjomba yupo kwenye nafasi Fulani atanisaidia kupata kazi, sio ajabu kusikia vijana vijiweni wakitambiana kuwa na ndugu kwenye nafasi za uongozi serikalini kwamba nikimaliza tu Anko, kaka, dada, shangazi, Baba mdogo watanivusha hata kama ufaulu ni mbovu as long as yupo ndugu nitakwenda...

Fikra tegemezi, ufungwa wa fikra, uliofungwa kwenye muujiza, ndiyo maana leo matapeli wa gospel wametapakaa nchi nzima kwa sababu asilimia kubwa tunaishi kwa kutaka kuwa watu fulani lakini uwezo wa kufikiri ukiwa mdogo tunawaza muujiza, bahati na sibu lakini na uchawa mwingi kwa wachache ambao wameamua kwa moyo wa dhati kujikomboa na kuishi ndoto zao...

Pingine tumeishi huko kwa muda mrefu sana, sio kwa sababu ya kizazi chetu bali ni mfumo na muundo ambao tumeukuta tangu zama zile. Mfumo wa zamani uliruhusu watu kuwa tegemezi kwa sababu ya kuwa na watu wachache waliokwenda shule, serikali na taasisi nyingi kuwahitaji watu kuliko leo tunavyohitajiwa na makampuni, maana tumekuwa wengi kuliko nafasi zenyewe....
Ni namna gani tunaweza kujikomboa kutoka kwenye hali ya kipato duni na kwend kwenye kiwango cha juu...

Kwanza kabisa nikuacha kuishi kwa kutegemea kuwa kuna siku nitakuja kupata ajira bali ishi kwa kusema ni namna gani nitayaishi maono yangu, iwe kwa ajira au kukosa ajira lazima niishi ndoto zangu. Ifungue akili na ufahamu wako, na kuanza kutazama na kufikiri upya, utaziona fursa nyingi ambazo tunazo katika taifa letu na bara zima la Afrika..

Ndoto za mwafrika zitatimizwa na mwafrika mwenyewe na ndoto zangu, ndoto zako zitatimilika kwa kuamua binafsi na si vinginevyo, maisha yetu leo ni maisha ambayo hayamhitaji mtu mwingine zaidi ya kujihitaji wewe mwenyewe kuamua kwa moyo wa dhati kwamba mimi ndiyo mwenye mamlaka yakujitoa hapa nilipo na kuwa mahali nataka kuwa..
Kila nikijitazama najiona mtu mkubwa lakini ili niwezd kufika mahali hapo juu, ni vyema kubadili mtazamo na fikra zangu juu ya uendeshaji wa maisha yangu, vivyo hivyo kijana mwenzangu unayo nafasi yakubadili hatima yako kwa nguvu na kwa maarifa yako...

Ufungwa wa fikra ni mbaya kuliko kawaida, aina hii ya kifungo huwa imewekeza zaidi katika kulaumu, kutaka kuwa chawa, kutegemea miujiza, kutegemea watu fulani nk. Hali hii hujenga majeraha na huzuni moyoni ambayo matokeo yake huondoa ufanisi katika utendaji wa kazi...

Vijana tunahitaji kubadilika sana, tunahitaji kuondoa matajirajio kwa watu bali tunapaswa kuwafanya watu waone (value)Thamani kwa kuja na mawazo mbadala katika kuhakikisha kuwa tunaondoka kwenye ufungwa wa fikra na kuwa watu huru. Mtu akishakuwa huru kifikra ni rahisi zaidi kuwa huru katika kufanya maamzi, kuwa huru katika kuchakata mawazo chanya yenye kuleta matokeo chanya. 

Vijana wenzangu, wazazi na kaka zetu ni vyema kuwa mabalozi wema kwa watoto wetu walau kuanza kuwaonyesha kuwa, uhuru wa fikra hutengeneza hali ya kujiamini, hali ujasiri sio unyonge tena, hii huwa ni nguvu ambayo inamfanya mtu kujitegemea kwa sababu ndani yake ipo nguvu ya kujisimamia na kutimiza malengo yake kwa ukubwa na upana....
Mtu akiwa huru kifikra ni rahisi zaidi kujisimamia, 
Moses_mgema 
0755632375

No comments:

Post a Comment