Wednesday, January 5, 2022

TWEKA MPAKA KILINDINI

Luka 5:4

Ni maneno ya Bwana Yesu akimwambia Simoni pamoja na wenzake hii ilikuja baada ya Simoni na wenzake kufanya kazi ya kuvua samaki usiku kucha wasiambulie chochote kile.

Tukio hili lilitokea katika ziwa la Genesareti alipokuwa akisongwa na watu na kisha akaanza kufundisha, ndipo alipomwambia Simoni Petro habari ya kushusha nyavu katika ziwa like tena katika kina kirefu (kilindini).

Yawezekana umekuwa katika kufanya kazi na matokeo yamekuwa madogo ukilinganisha na kipato unachopata.

Hivyo kama wewe ni mmoja wapo somo hili litakufaa sana, vilevile kama mambo yako yanaenda vizuri linakuhusu pia kwa ajili ya kesho yako ambayo ni fumbo.

Ukitafakari habari ya Yesu na makutano pale kwenye ziwa la Genesareti utaona Bwana Yesu, alikuwa akihangaika sana katika kuwafundisha makutano, yale mazingira yalikuwa ni magumu sana kutokana na kwamba watu wengi walimsonga na yeye alitaka kuwafundisha zaidi katika utulivu, hivyo hakuona kama akiendelea katika hali ile ile atatimiza kusudi lake, ndipo akaamua atafute madhabahu ya kuwakutanisha wale watu pamoja, mahali atakapotulia ili awafundishe wale watu katika ustaarabu na utaratibu ambao Mungu ameukusudia..

Na alipogeuka akaona vyombo viwili vimeegeshwa pwani na wenye navyo wametoka, ndipo akikichagua cha mmojawapo na kukigeuza kuwa madhabahu yake ya muda.

Sasa Chombo kinawakilisha nini katika mazingira tuliyopo leo?. Chombo kinawakilisha kitu chochote cha kujipatia kipato, kumbuka chombo hicho Bwana alichokitumia kilikuwa ni cha akina Petro cha kuvulia samaki, kwasasa hivi chombo kinaweza kikawa, elimu ya mtu, ujuzi wa mtu, biashara ya mtu, fremu ya mtu, shamba la mtu, kiwanja cha mtu,n.k.

Lakini tunasoma katika habari hiyo, tunaona Bwana alipotazama hakuchagua vyombo vilivyokuwa kando kando vyenye wavuvi au samaki, kumbuka vilikuwepo tu vingi vizuri zaidi ya hivyo vilivyokuwa vinazungukazunguka maeneo yale, lakini yeye hakuchagua chochote kati ya hivyo bali alivichagua vile visivyokuwa na kitu ndani yake…(Na ndio maana somo hili linawahusu sana wale ambao shughuli zao haziendi sawa),

Sasa kilichotokea ni kwamba wakina Petro walifanya kazi ya kuchosha usiku kucha wakihangaika kutafuta samaki ukanda mzima wa ziwa la Genesareti kwa shida, na kujitoa kweli kweli lakini wasipate kitu, mpaka kulipokucha wakakata tamaa ya kuendelea kuvua tena, wakaona kilichobakia tu ni kukipumzisha chombo na kuzitengeneza nyavu zao tena, kisha kuzihifadhi mpaka wakati mwingine,

Lakini baadaye kidogo ndio tunamwona Bwana Yesu akisumbuka na wale makutano, ndipo wao wakamruhusu Bwana kutumia vile vyombo ili kutimiza kusudi lake la kuhubiri,. Na baada ya Bwana kumaliza kuhubiri, sasa wakati makutano yote wameshaondoka ndipo akawageukia wale wamiliki wa vile vyombo, na kuwaambia twekeni mpaka kilindini mkashushe nyavu zenu mkavue samaki.

Lakini wao walimwambia, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha pasipo mafanikio, na walipokubali tu kwenda kuvua walipata matokeo makubwa ya kushangaza, mpaka nyavu zao kuanza kukatika, mpaka kufikia hatua ya kuomba msaada kwa wingi wa Baraka hizo, maana zimekuwa nyingi mpaka kushindwa kuvuta zile nyavu kutokana na wingi wa samaki ikalazimisha kuomba msaada kutoka katika chombo cha pili, maana wingi wa samaki ulipelekea chombo chao kuanza kuzama ndani ya maji ya ziwa.

Yesu ni yeye Yule jana, leo na hata milele hajabadilika, leo pia anaweza kufanya kama alivyo fanya kwa Simon petro na wenzake.  Umejaribu kufanya mambo mengi kwa bidii na ufanisi mwingi lakini kwa bidii, lakini bado huoni matokeo yanayoendana na bidii yako

Leo hii hicho chombo chako kigeuze kuwa MADHABAHU YA KRISTO kwasababu anakitafuta hicho ili alifanye kusudi lake, kumbuka pale Yesu hakutafuta sinagogi la kuwakusanya wale makutano waliokuwa wanamsonga, hakutafuta hekalu, wala hakutafuta mahali patakatifu bali alitafuta MAHALI PA KUJIPATIA KIPATO KWA MTU, mahali ambapo mtu anapopategemea kujipatia mkate wake wa kila siku, na pia fahamu tu, siku zote Bwana anapaangalia mahali ambapo palipo patupu kama kwako wewe, Mahali ambapo pamefanyika kazi ya kuchosha miaka mingi, miezi mingi pasipo mafanikio yoyote, hapo ndipo anapopataka kwa ajili ya kazi yake, na akishamalizana napo hapo, ndipo atakwambia nenda katupe nyavu zako kilindini uvue samaki, kwa wingi wa atakachokupa Bwana utaita mpaka na marafiki na zako na maadui zako waje nao kushiriki Baraka zako Mungu alizokuandalia.

Leo Kazi yako wewe ni ya ufundi, una ujuzi wa kutosha kuhusu masuala ya ujenzi, na unaona mahali unapofanyia pengine ni kanisani kuna kasoro Fulani ya ujenzi, na shughuli zako za kijenzi haziendi sawa, umekuwa ukipata mapato kidogo kupitia hiyo,wakati mwingine unakosa kabisa kazi, huo ndio wakati wa kwenda kumruhusu Bwana atumie hicho chombo chako (ujuzi),

nenda mahali unapokusanyika (kanisa), kazi ya Mungu inapofanywa, angalia kasoro zinazohusiana na taaluma yako, na utumie ujuzi wako kurekebisha tatizo hilo bila kutazamia malipo yoyote, pengine umeona ukuta wa kanisa umebomoka au una ufa, uzibe, umeona mfumo wa maji haujakaa sawa na una ujuzi wa kufanya hivyo, urekebishe hata kama hauna chochote, umeona kanisa halina choo kinachostahili, na wewe una ujuzi wa namna ya kutengeneza vizuri, nenda kafanye hivyo, kajenge kwa ustadi wote, na maarifa yako yote, umeona kuna kasoro ya umeme na mfumo wa nyaya, na una ujuzi huo nenda karekebishe usisubiri hata mtu akamwambie, mruhusu Bwana atumie hicho chombo, na mwisho wa siku utaona matokeo na mtu asiyefanya hivyo wakati Fulani ukifika.

Au wewe ni polisi au mlinzi, anza kutoa mchango katika sekta hiyo ndani ya kazi ya Mungu..Usiseme Mungu kweli ataweza kutumia taaluma hii/ujuzi huu kwenye kazi yake??..kumbuka Yesu alitumia mtumbwi wa wavuvi kuwapelekea maelfu ya watu katika ufalme wa mbinguni…Na wewe vivyo hivyo mpe Bwana chombo chako.

Au wewe unafanya kazi ya upishi, na unaona kazi zako haziendi sawa, faida ndogo, na unaona kuna uhitaji mkubwa wa wapishi ndani ya nyumba ya Mungu, labda kwa ajili ya wazee wasiojiweza (wakristo), au wageni, au wenye mahitaji na mayatima (walio wakristo), ndani ya kanisa n.k usingoje uambiwe au uwe na kitu kwanza ndio ufanye, wewe mwenyewe anza kuchukua hatua ya kujitolea kwenda kuifanya, tena pasipo hata kuombwa.

Wewe ni mtengeneza bustani, na ndiyo kazi yako umekuwa ukifanya kwa ajili ya kujipatia kipato..Lakini mazingira ya kanisani ni machafu au hayavutii, panaonekana ni mahali pasipo tofauti na sehemu nyingine yoyote, Tumia chombo chako (ujuzi) kurekebisha mazingira ya Mungu, pakavutia kama vile unavyopendezesha bustani za watu wengine,..unaweza ukaona ni jambo dogo lakini linamaana kubwa na Bwana akisharidhika atakuambia shuka vilindini..utaona milango Mungu anayokufungulia katika hiyo hiyo kazi yako ilivyo ya ajabu.

Wewe ambaye ulikuwa unatafuta kazi,na bado hujapata, angali unao ujuzi Fulani, usiuache ulale utumie huo ujuzi katika kazi ya ufalme wa mbinguni, kwamfano labda wewe ni “ IT ” (mjuzi wa katika teknolijia ya Kompyuta), unaweza uka unda wavuti na tovuti kwaajili ya kutangaza ufalme wa mbinguni, unaweza ukabuni programu za kutangaza kazi ya Mungu kirahisi katika mitandao fanya kiuaminifu kabisa..Na Bwana akishamaliza kutenda kazi kwa kutumia chombo chako, atakuambia shuka vilindini…Utaona nafasi ambayo ulikuwa unaitafuta kwa kuhangaika kwa muda mrefu pasipo mafanikio kama wakina Petro walivyokuwa..unaipata ndani ya kipindi kifupi tena chenye faida mara 100 zaidi ya kile cha mwanzo ulichokuwa unakihangaikia..

Lakini hizo zote zinakuja kwanza kwa kumtolea Bwana chombo chako akitumie, kwa ajili ya kazi yake, lakini kuna wengine hawapendi kumpa Bwana nafasi lakini wanataka Baraka za Bwana, utakuta mtu analo eneo kubwa limekaa pasipo matumizi yoyote, hataki hata kukaribisha watu wafanyie kazi za mikutano ya injili hapo, na bado anataka Mungu ambariki, ndipo hapo zile roho za udanganyifu zilizoachiliwa katika siku za mwisho zinaanza kumdanganya na kumshawishi, akanunue mafuta ya upako, anunue chumvi na maji ya Baraka akanyunyuzie kwenye kiwanja chake na kwenye biashara yake, aanze kukemea roho za laana katika kiwanja chake, au biashara zake, ili mambo yake yaanze kwenda vizuri.

Utamkuta mwingine anazo fremu za vyumba na zimekosa mpangaji wa kufanyia biashara au tution,..na wakati huo huo kuna wakristo wenzake wamekuja kumwomba awape angalau fremu moja wawe wanafanyia bible study au maombi wakati wa jioni kwa muda huku wanatafuta eneo lingine..lakini kwasababu hajui uweza wa Mungu, anawazuilia na kuona bora tu ziendelee kuwa zimefungwa.na wakati huo huo anazunguka kutafuta kuombewa na kununua maji na mafuta ya upako huku na kule hata wakati mwingine nchi na nchi..Mtu wa namna hii hawezi kutazamia miujiza kama waliofanyiwa wakina Petro.

Bwana anasema nikaribieni, nami nitawakaribia… Wakati mwingine kutokuwa full committed  katika eneo lako la utumishi umekuwa chanzo cha kazi ya  Mungu kuwa katika hali dhaifu na wewe hutaki kuifanya chako..(Hagai 1:1-12). 

Anza leo kufanya kama Simoni Petro alivyofanya na wenzake na Mungu atakubariki. Mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.

Tutaendelea na somo hili baadae......

Moses Zephaniah Mgema

moses@gmail.com 

No comments:

Post a Comment