Sunday, April 28, 2019

FAIDA YA KUWA MWAMINIFU

Mtu kumwamini mtu inaweza kuwa ngumu sana. Hii inatokana na baadhi ya watu kutendwa vibaya na watu ambao awali walijenga imani kwao lakini walioamini wakafanya kinyume na vile walitarajiwa kuwa hapo awali.

Kadri miaka inavyokwenda jambo kuaminika kwenye jamii limekuwa likipungua kila siku, kuanzia kwenye mahusiano ya ukoo, familia, ndugu jamaa na marafiki, mahusiano ya kimapenzi, na mambo mengine mengi ndani ya jamii yetu Tanzania hata duniani kwa ujumla.

Watu wengi wamepoteza uaminifu sana kwa sababu ya tabia yakutokuwa waaminifu, mtu anaweza akapewa pesa, au akatendewa jambo Fulani lakini mwisho wa siku matokeo yake yanakuwa hasi ambayo ni kinyume na matarajio

Jambo limetokea hata kwenye ngazi za kitaaluma, makazini, hata kwenye maeneo ya dini ambayo kwa kifupi yalikuwa ni maeneo yaliyoaminiwa na kuaminika zaidi ndani ya jamii.

Yapo mambo mengi yanachangia hali hii kutokea lakini mwisho wa siku hitimisho lake ni kwamba tabia ni hali ambayo mtu akiiendekeza inaweza kuwa sugu na kuathili moja kwa moja mfumo mzima wa maisha yake.

Ubinafsi, kutokufanya kazi, mazoea, kuuma kwa roho unapotaka kurejesha fedha ya uliyokopa, kujiendekeza na tabia Fulani, ulevi, udokozi, maisha ya kijamaa kutawala, kutokuthamini kitu au jambo la mwenzako, ubabe, utani uliovuka mipaka, kukosa hekima na busara, ugumu wa mioyo na kuishi maisha bandia ambayo hayana uhalisia na maisha halisi ya kwako hivyo watu vile wanakutazama na uhalisia wako ni tofauti kabisa, kutokuwa wakweli na kutumia njia za uongo ili kukidhi haja ya mahitaji yetu.

Hizi ni baadhi ya tabia ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza uaminifu kwa watu wengi bila kujua madhara ya kukosa uaminifu kwa watu, jamii hata maeneo ya kitaaluma na maofsini ambapo tunafanya kazi kwa kuajiliwa au kujiajiri.

KATIKA SOMO HILI TUTAJIFUNZA MATOKEO CHANYA YAKUWA MWAMINIFU KATIKA JAMBO LOLOTE.

Hakuna jambo jema kwa mtu kama kuwa mwaminifu yeye mwenyewe binafsi, kwa wazazi wake, watoto, kazini, kanisani/msikitini na kwenye jamii kwa ujumla. Zifuatazo ni faida za kuwa mwaminifu.

1. Kuaminika zaidi
Moja ya faida kubwa ya uaminifu ni jamii kukuamini, kazini, kwako au kwa wateja wako na kama wewe ni mfanyabiashara na ni mwaminifu kwa wateja wako, unafungua kwa wakati, unawahudumia vizuri kwa lugha mzuri na yakupendeza, bei sio za ubabaishaji, mtu akiacha pesa yake anaikuta, basi utajijengea idadi kubwa ya wateja kwa sababu ya uaminifu wako wao kwa wao watapeana taarifa zako,

2. Hujenga mahusiano imara na bora.
Ukiwa mwaminifu kwa jambo lolote lile lazima mahusiano yako na watu yatakuwa mazuri, iwe ni kazini, shuleni, kwenye nyumba za ibada, kwenye sehemu za mahitaji na sehemu nyingine nyingi hutasikia migongano na lawama kutoka kwa watu husika ambao labda unafanya nao kazi, bosi wako, walimu au wanafunzi, ndoa yako nk. Maeneo hayo yote yatakuwa bora na imara hivyo uaminifu ni jambo nyeti sana na ni vyema kulitilia mkazo na kulitimiza.

3. Huimarisha ushirikiano.
Mtu mwaminifu huwa na ushirika mzuri na watu wenzake, mfano wewe kama ni boss kuwalipa wafanyakazi wako kwa wakati, kutimiza ahadi zako au mzazi kutimiza ahadi unazoahidi kwa watoto au mke hii inatoa motisha na ushirika mzuri toka kwa wafanya kazi au kwa watoto kumfurahia baba au mama yao. Vile vile hata wafanyakazi wakitimiza kazi zao kwa uaminifu ushirika huwa ni mzuri kati yao na kiongozi wao. Na maeneo mengine ambayo sijayataja kama mifano hai kwenye maisha yetu.

4.Utapewa nafasi zaidi.
Hii hutokea kwenye jamii, makazini na hata nyumbani. Unapokuwa mwaminifu ndipo nafasi ya kupewa nafasi zaidi iwe ni kazini, nyumbani kwa wazazi basi nafasi hizo huwa ni kubwa na hata maeneo mengine mengi.

5.Utakula vya sirini.
Mtoto mtii na mwaminifu kwa wazazi wake hula vya uvunguni kwa sababu huyu mtoto hutekeleza majukumu yake kama mtoto vyema bila kusukumwa wala kubembelezwa na anajua wajibu wake. Ndivyo hivyo hata kwenye familia, jamii kwenye biashara, kazini  ni rahisi kushirikishwa mambo makubwa ya kiofsi kwa sababu wanajua wewe ni mwaminifu katika kutimiza, kutekeleza na kutunza siri za kampuni vyema hivyo ni rahisi kupata taarifa mapema.

6.Ni rahisi kusaidika.
Mtu mwaminifu huwa anatengeneza mazingira mazuri ya kupata msaada kwa haraka either wa kifedha, kimawazo au msaada wowote ule sababu kubwa ni ule uaminifu aliojijengea kwenye mazingira  yake ya maisha, iwe kwenye biashara, benki, nyumbani, kazini na maeneo mengine mengi ambayo yanamhusu.

7.Ni njia bora ya kuimarisha ndoa na mahusiano

Hakuna kitu kizuri kwenye mahusiano au ndoa kama uaminifu. Uaminifu ni ufunguo wa furaha ndani ya ndoa, ni ufunguo wa mafanikio na Uhuru wa nafsi, ufunguo wa kuyaona mahusiano  au ndoa yako ni ya maana kuliko zingine na kuongeza thamani ya penzi lenu ambalo litastawi na kuchanua vyema. Hivyo uaminifu kwenye mahusiano na ndoa ni msingi imara.

8. Utatetewa wakati wa Magumu au mapito.

Changamoto kubwa kwa watu ni kutokuimarisha mahusiano yao na watu wengine kwa njia ya amani, waonevu, wadhurumaji, kufanya mambo bila kujua kuna kesho ambayo inaweza kuwa na uhitaji wa wale watu unaowatendea ndivyo sivyo. Mtu mwaminifu hujiongezea nafasi ya kutimiza malengo yake kwa sababu ukifanya kwa uaminifu kwa watu basi watu hao hao kuna wakati watakuwa daraja lako la kufikia jambo Fulani maishani mwako, katika uonevu utapata watetezi wengi.

9. Mtu huishi kwa amani na furaha.
Mtu mwaminifu huishi kwa furaha, amani lakini pia huwa na upendo, hapendi kuiona nafsi yake ikisononeka, ikiumia kwa kuidhurumu kwa kukosa uaminifu, hupenda kutenda jambo kwa wakati na uaminifu kwa wengine. Kutokana na kufanya mambo hayo kwa uaminifu basi moyo na akili yake hubaki huru bila deni maana amefanya kila jambo kwa wakati na uaminifu.

10.Uaminifu ni dawa
Huondoa msongo wa mawazo, humfanya mtu kuwa huru asiye na hatia, kumbuka mtu asiye mwaminifu huishi kwa uongo, muda wote anatengeneza mazingira ya kuutetea uongo wake na kuuhalalisha bila kujua kuwa anajiumiza binafsi, anatumia nguvu nyingi kupanga namna ya kudanganya wakati kama angeamua tu kuwa mwaminifu nguvu ile ile  angetumia kwa ajili ya kufanya jambo lenye maana maishaini

Kwa hiyo ni vyema kutengeneza mazingira ya kuaminika na wazazi, watoto, mke, mume, jamii, na katika maeneo yote unayokuwa.
Kwa sababu uaminifu hutengeneza mahusiano mazuri na kuaminika na watu, na kama basi ikitokea kuna fursa inatokea watu watakufikiria na kukupa nafasi.
Prepared by..
Moses Zephania Mgema
0715366003/0755632375
Email mgemamoses@gmail.com
Dar es salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment