Tuesday, August 9, 2022

MALEZI, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UTAMADUNI WA MWAFRIKA

Malezi ya watoto na vijana katika ulimwengu wa sasa imekuwa ni changamoto kubwa sana katika nchi yetu na bara zima la Afrika, hii inachangiwa na kiwango kikubwa cha mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yanapelekea mwingiliano wa tamaduni kutoka taifa moja kwenda taifa jingine na bara moja na bara jingine...

Mwingiliano huu umekuwa ukichagizwa sana na dunia kuwa karibu sana na maisha ya watu kuliko namna ambavyo watu wa dunia ya tatu tulitegemea kwa kipindi kifupi namna hii, ndiyo maana kumekuwa na mapokeo tofauti tofauti na mitazamo tofauti tofauti juu ya uwepo huu wa mwingiliano wa kitamaduni na mila kutoka maeneo tofauti ya dunia yetu.

Mwingiliano huu wa kitamuduni na mila haujaletwa tu na kuhama hama  kwa watu kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, njia ambayo kwa miaka mingi ndiyo ilikuwa inaleta mwingiliano wa watu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine na lengo kuu lilikuwa ni kutafuta fursa za kibiashara zaidi kuliko miaka hii ya karne tuliyo nayo...

Mwingiliano umekuwa mkubwa kwa sababu ya sayansi na teknolojia ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa watu kupata taarifa kwa ukaribu na uharaka zaidi kupitia viganja vya mikono yao, mfano leo tuna Television na radio za mikononi, YouTube, mitandao ya kijamii ambayo imerahisisha watu kujifunza na kuona mambo mengi kupitia njia rahisi kabisa za upatikanaji wa taarifa zote ambazo mtu anahitaji kwa muda anao taka.

Kuwepo kwa mwingiliano huu wa tamaduni, desturi na mila, haujaanza leo, haujaanza leo kwa sababu mabadiliko ya duniani yamekuwa yakitokea tangu karne ya kwanza, hata leo, dunia ikipewa vifaa rahisishi zaidi ambavyo vinampa mwanadamu nafasi ya kurahisisha majukumu yake na kuyafanya kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na enzi za kale.

Katika bara la Afrika malalamiko yamekuwa mengi zaidi hasa kutoka kwa wazazi na walezi, ambao kwa asilimia kubwa ni kama hawakujiandaa kuyapokea matokeo haya makubwa ya teknolojia, wengi wakisema kuwa mila, desturi na tamaduni za mwafrika zinaharibiwa na utamaduni wa kimagharibi, hii ni kutokana na tamaduni hizi kuwa na nguvu zaidi ukilinganisha na utamaduni wa mwafrika.

Wakati sisi tunapokea utamaduni wa kimagharibi, hatukujua kuwa tunaupokea, tulijua ni misaada na usaidizi wa kimaisha kumbe ndiyo tulikuwa tunatengeneza mazingira ya kukubali kuwa wanyonge, na daraja la mtawala na mtawaliwa lilikuwa linajengeka katika fikra ambazo kwetu hazikuwa tunduizi bali tulitazama misaada kwa wakati huo.

Miaka mingi nyuma kabla ya ukoloni, historia inaonyesha kuwa Waafrika walikuwa tayari wameshasogea katika ugunduzi wa vifaa mbalimbali ambavyo vilikuwa vinatumika katika kuwarahisishia utimizaji wa majukumu yao kwa kipindi hicho, tunaona ugunduzi wa moto, ugunduzi wa vifaa vya kilimo na Silaha na nyenzo nyingine nyingi ambazo zilikuwa zikitumika katika kuwarahisishia mambo yao..

Kuja kwa ukoloni ndipo changamoto ya kuruhusu mwingiliano wa kitamaduni ulipoanzia rasmi, na katika kipindi hicho utamaduni kutoka mabara mengine ulianza kuwa na nguvu zaidi kwa sababu tuliaminishwa kuwa tamaduni zetu zilikuwa na mahusiano ya kichawi na uabuduji wa mizimu isiyo na tija, hivyo walituletea utamaduni mpya ili kutustarabisha, kutokomboa na kutupa maisha mapya ambayo sio ya gizani kw akifupi walikuja kuleta mwanga katika giza...

Kwa hiyo tunachokiona leo ni matokeo ya michakato mingi ambayo ilianza karne nyingi nyuma mpaka kufika leo. Sasa kutokana na kukuwa kwa sayansi na teknolojia umekuja kukamilisha kazi ambayo ilikwisha kuanza siku nyingi na kwa sababu kama bara la Afrika tumeshindwa kujisimamia wenyewe kuanzia ngazi za utawala, biashara, matibabu na kiimani kwa muda mrefu ni vyema sasa kutambua kuwa sio rahisi kupingana na mabadiliko makubwa ambayo kwa asilimia kubwa sana yanachagizwa na ukuaji wa teknolojia...

Kupiga na kuona utamaduni wa kimagharibi kuwa ni mbaya leo sio sawa kwa sababu udhibiti wake ni mgumu sana, tunachopaswa kufanya sasa ni kuhakikisha kama nchi au bara linasimama kwa kujitegemea katika mambo ya uendeshaji wa mambo yake. Lakini je tuna hiyo nguvu ya kujitegemea kwa sasa au tutasubiri kwa miaka mingi zaidi ya hii tuliyoishi baada ya uhuru ?...

Mambo haya yanatokea leo kwa sababu ya kuongezeka kwa kitu kinaitwa mmomonyoko wa maadili hasa kwa watoto na vijana ambao wamekuwa wahanga zaidi wa mwingiliano wa tamaduni hizi kwa njia ya teknolojia. Kwangu mimi hii sio hoja kubwa sana kwa sasa, kwa sababu tumeshachelewa na udhibiti wake ni unategemea zaidi katika udhibiti wa mifumo ya kimitandao ambayo haitawapa watu access ya kupata taarifa wanazotaka kwa wakati wao bali iwe katika utaratibu wa kiinchi kama ambavyo baadhi ya nchi za kiarabu na baadhi ya nchi za Asia kuwa na mifumo yao inayojitegemea hivyo kuwa na uwezo wa udhibiti katika kuperuzi katika mitandao ya kijamii.

Lakini lazima tutambue kuwa kuishi kwenye utamaduni wa mwafrika pekee sio tija wala hakuna manufaa yeyote katika ulimwengu ambao tuko nao leo, leo nchi haiko katika uendeshaji wa mambo kwa mfumo wa kijamaa, kila mtu yupo na uhuru wa kufanya mambo yake mwenyewe, utamaduni huu wa kimagharibi hautulazimishi kuishi wao wanavyotaka bali sisi wenyewe tumeupokea na tunaufurahia sana kuliko hata wao kwa upande mmoja...

Lakini bado wanatuonyesha madhaifu mengi sana katika matumizi ya teknolojia, wenzetu wakitumia kwa manufaa makubwa ya kibiashara, na kazi sisi tumezigeuza platform hizi kuwa sehemu za kupeana mipasho na kuwekana wazi mambo yetu kwa maana ya taarifa za udaku..

Tutakuwa na mwendelezo wa kuelezea zaidi kiini cha lengo la makala hii katika toleo lijalo...
Moses Zephania Mgema 
0719110760, 0755632375
mgemamoses@gmail.com 
mosesmgema12.blogspot.com
moses_mgema on Instagram, twitter and Facebook 

No comments:

Post a Comment