Katika safari ya maisha kuna namna mtu huchagua kuishi hasa kwenye eneo la tabia na kiukweli kabisa tabia ya mtu ndiyo picha ambayo watu wanaweza kuitumia kwa ajili ya kumwelezea huyo mtu na watu hawawezi kusema tofauti na mtu ambavyo anaishi na kubahave.
Na katika mfumo wa maisha yetu kuna aina mbili tu za tabia ambazo zinatumika kumtambulisha mtu kwa watu au ndiyo alama ya utambulisho wake kwa watu wanaomfahamu.
1. Tabia njema
2. Tabia mbaya
1. Kwenye Tabia njema : Ni mkusanyiko wa mambo yote chanya ambayo mtu anayafanya kwa ajili yake na kwa ajili ya wengine mfano mtu akiwa ni mtu wa ibada, anafanya kazi kwa bidii, mwaminifu, mwenye huruma, kusaidia wengine, kuchukulia mambo katika mtazamo chanya hata kama kuna namna ameumizwa lakini anafikiri lengo la kwanza kabla ya mtokeo haya ilikuwa ni nini, mkweli mwenye upendo, mwenye nia ya kujenga na kuboresha zaidi kuliko kuharibu na kuumiza nk. Hiyo inaweza kuwa ni tabia njema sana.
2.Tabia mbaya: Ni tabia ambayo ndani yake huwa na malengo maovu tu hata kama kwenye sura ya nje inaonekana ni mambo mazuri mfano kutumia nafasi tulizonazo vibaya, kubana haki za wengine kwa manufaa binafsi, kuumiza wengine kwa sababu ya nafasi uliyo nayo, chuki bila sababu ya msingi, kuwa na wajibu wa jambo fulani lakini hufanyi na unajua ukifanya wengine pia watanufaika, uchoyo, kukosa utu, rushwa, fitina na mambo mengine yafananayo na hayo. Hayo yote yanaingia kwenye kundi la tabia mbaya.
Rafiki yangu yote ambayo nayafanya mimi leo au unayafanya wewe leo fahamu tu kuwa hiyo ni mbegu na ipo siku mbegu hiyo itaota na kustawi vyema kabisa whether ni mbegu ya magugu au mbegu ya ngano bora.
Baada ya Baba yangu mzazi kuondoka duniani baadhi ya marafiki zake wengine ambao hata tulikuwa hatuwajui walikuja nyumbani, wengine tulikuwa tunakutana nao njiani wanasema hivi kwa maisha ya Baba yenu na namna ambavyo aliwekeza mambo mema kwa watu basi hamwezi kuishi kama yatima hata siku moja.
Kijana mmoja ambae kiumri yeye kwangu ni mkubwa tu tukakutana nae akaulizia habari za mzee wangu nikamwambia mzee amesharudi mbinguni kwa Baba alissikitika sana lakini akasema Baba yako alinitendea jambo hili na hili wakati maisha yangu bado yako gizani siwezi kumsahau kabisa na mimi ndiyo kaka yako wa hiari tangu kipindi hicho hadi leo amekuwa kaka kweli kweli ila ni kwa sababu ya Baba yangu.
Wapo wengi sana ambao kwa wema na uzuri wa mzee wangu leo hii singida imekuwa zaidi ya nyumbani kwetu Kahama, tulijua pengine baada ya mzee kufariki tungerudi nyumbani kwa sababu tu tuko pekee yetu singida na tulikuja singida kwa sababu ya kazi ya Baba pia lakini kitu kilichotubakisha Singida ni wema wa mzee wangu kwa watu.
Nakumbuka siku moja Baba aliwahi kuniambia hivi, watendee watu wema, maana hiyo ni roho ya Mungu, fikiria dhambi za Adamu pale edeni lakini uchukue moyo wa Mungu baada Adamu na Hawa kukosea nini kilitokea, baada ya maneno hayo akamalizia kwa kusema hivi.
Mbegu ya wema inaweza kuchelewa kumea kwa sababu ubaya na uovu una nguvu katika sura ya nje lakini kwa sababu wema huwa una nguvu ya ndani na mizizi yake ni
1. Upendo
2. Utu
3. Amani
Basi hata kama utaonekana kwa sura ya nje ni dhaifu ipo siku moja nguvu yake itaonekana katika matokeo ya matendo yake, Mungu alikasirika sana, alichukia sana kwa makosa ya watu ambao aliwaamini, walimwangusha lakini mwisho wa siku nguvu ya upendo, Thamani, Mungu aliona hakuna kitu naweza kufanya zaidi ya kusamehe na kuanza upya na ndiyo matokeo ya ulimwengu tulio nao.
Baba amelala lakini watoto wake tunakula matunda ya matendo yake kwa watu ambao kwa asilimia kubwa sio ndugu zetu, sio watu wa kabila moja na sisi wala si watu tunaotoka nao ukanda mmoja, sisi sio matajiri kwamba watu wanatupendea utajiri wetu, wala baba hakuwa tajiri bali alikuwa na moyo wa upendo na utu sana.
Mzazi/Mlezi/kiongozi, Boss, mwajiri jifunze kuwatendea watu mambo mema, waelekeze, waonye kwa nia ya kujenga sio kukomoa, saidia watu kama unajua sio kujifanya mjuaji kwa lengo la kuumiza wengine.
Kama ambavyo mbegu njema yaweza kuota na kuleta matokeo basi fahamu hata mbegu ya uovu huota na kuleta matokeo yake pia. Tofauti ya matokeo ya hizi tabia mbili moja hunufaisha hata kizazi chako bali nyingine inaweza kuwa chanzo cha kuumiza kizazi chako ukiwa wewe umelala.
Jifunze kuishi vyema, matendo yako yawe yenye lengo la kujenga zaidi kuliko kuangamiza, hakuna faida utapata ukimuumiza huyu wala hakuna tuzo ya kuwaumiza wengine bali unachimba kaburi la watoto wako na kizazi chako cha kesho.
Kuna vijana wanapitia magumu kwa sababu ya wazazi wao, wanakosa nafasi kwa sababu ya tabia za wazazi wao, watu wanasema watu wa ukoo huu ni wabaya sana mkiwapa nafasi itakuwa kama baba yao alivyokuwa, masikini ya Mungu kizazi chako kinaumia kwa sababu ya matendo yako mabaya.
Kuna nafasi ya kubadilika, uyafanyao leo sio ujanja, wala haimanishi wewe una akili nyingi kuliko wengine, hata ambayo unayafanya kwa siri, unawaficha wanadamu lakini Mungu aonae sirini anajua na ipo siku matokeo ya maamzi ya kuumiza watoto wengine itazaa matunda tu hasa kama hatotokea mtu hapo katikati wa kuvunja hiyo chaini ya chuki na ukatili dhidi ya wengine.
Saidia watu kwa lengo chanya, onya watu, adhibu watu kwa lengo la kujenga sio kukomoa, duniani tunokosea hakuna mkamilifu duniani ila tunasaidiana kwa upendo ili kuendelea kutunza amani na furaha zetu.
Chagua leo ni mbegu ipi bora kwako kati ya hizi mbili ?
No comments:
Post a Comment