ELIMU YA PADRE WA KANISA KATOLIKI
(Sehemu ya Tatu)
Na. John-Baptist Ngatunga
___________________________
Sifa za Kipee za Viongozi wa Kanisa Katoliki:
1. Baadhi ya Sifa hizo ni kwamba, Viongozi hawa kwa kawaida huwa hawahangaiki na Vioja; wanahangaika na Hoja. Ukija na Hoja watakujibu kwa Hoja; ukija na Vioja wala hawakuhoji. Wanajibu Hoja kwa Hoja sio Hoja kwa Vioja.
2. Mfumo wao wa kutatua changamoto daima huwa ni Majadiliano zaidi kuliko Mabishano. Hawawezi na hawapendi kubishana, ila wanapenda kujadiliana. Hii ni kwasababu wanajua kuwa kubishana ni kutaka kujua nani yuko sahihi ila kujadiliana ni kutaka kujua nini kipo sahihi.
3. Wanapenda kucheza na Masuala (Issues) sio watu. Wanajadili Masuala hawajadili sana Matukio au watu. Ndio maana hata linapotokea jambo la Kitaifa kama hili suala la Mkataba wa Bandari kati Tanzania na DP World waliongelea suala lenyewe yaani MKATABA na wakajikita katika Hoja hiyo. Hawajamlenga Mtu au Watu. Wamezungumzia Mkataba (Issue) sio Watu na Dini zao au Makabila yao.
4. Hawana desturi ya kukurupuka katika Maamuzi yenye maslahi mapana kwa Jamii. Wanajipa muda wa kutosha kulitafakari jambo, kusali na kuliombea Taifa au Jamii, kufanya Tafiti juu ya jambo kabla ya kutoka hadharani na matakamko. Ndio maana wakitoa WARAKA au TAMKO unakuwa Mjadala wa Kitaifa. Na ndiyo desturi ya Wanafalsafa (They don't rush to conclusion without premisses).
Tofauti na baadhi ya Taasis ambazo hukurupuka tu kama chafya na kutoa matamko bila kufanya Tafiti. Wakati mwingine badala ya kujikita katika NINI, wao wanajikita katika NANI. Badala ya kujibu Hoja kwa Hoja wenyewe wanawashambulia watoa Hoja. But it's not to the Catholic Church.
5. Kwa kuzingatia historia ya Maisha yao ya Kitaaluma, usomi, akili, upeo na uelewa mkubwa walio nao; itoshe tu kusema kuwa Kanisa Katoliki ni moja ya Taasisi zinazoongozwa na Viongozi wenye Matumizi mazuri sana Akili. Na kwamba 'Intelijensia' ya Kanisa Katoliki huwa haibabaishi, haibahatishi, haikisii, haikurupuki, haionei, haidanganyi. Ipo objective na inatenda haki.
6. Na kutokana na hilo sitakuwa nimekosea nikisema, "The Catholic Church is the Big Brain Institution; Full of Competent, Confident and Confidential Intellectuals led by the Power of the Holy Spirit to lead God's people bodily and Spiritually" (Kanisa Katoliki ni Taasisi yenye Akili kubwa; iliyojaa Wasomi Mahiri, wanaojiamini na wasiri wanaoongozwa na Nguvu ya Roho Mtakatifu kuwaongoza watu wa Mungu Kimwili na Kiroho).
7. Viongozi hawa ni Watu wenye Moyo wa kusaidia sana Jamii kwa kutoa Huduma mbalimbali za Kijamii ili kuiinua Jamii kutoka Lindi na Tupe la Umasikini. Angalia Huduma za Kijamii zitolewazo na Kanisa: Elimu, Afya, Maji, Nishati ya Umeme, Ajira, na nyingine nyingi.
8. Hawa Viongozi wakiliamua jambo lao, ni lazima tu litafanikiwa kutokana na umakini, umahiri, uchapakazi, kujitoa, uadilifu, Imani. Angalia Jinsi Taasis za Elimu na Afya wanazozianzisha, kuzisimamia na kuziendeleza zinavyofanya vizuri: Angalia Vyuo Vikuu kama:
(i) St. Augustine University of Tanzania (SAUT)
Pamoja na Vyuo vyake Vishiriki vyote
(ii) Ruaha Catholic University (RUCU)
(iii) Catholic University of Health and Aliened Sciences (CUHAS -BUGANDO)
(iv) Mwenge Catholic University (MWECAU)
Sijavitaja Vyuo vya Kati, Seminari Ndogo na Shule za Sekondari ambazo zinafanya vizuri sana Kitaifa na Shule za Msingi.
Angalia pia Hospitali mbalimbali:
(i) Hospitali ya Rufaa Bugando (Mwanza)
(ii) Hospitali ya Peramiho (Ruvuma)
(iii) Hospitali ya Ndanda (Mtwara)
(iv) Hospitali ya Ifakara (Morogoro)
(v) Hospitali ya Lugarawa (Njombe)
Zijavitaja Vituo vya Afya na Zahanati.
Na kwa hapa Tanzania ukiiondoa Serikali katika suala la utoaji wa Huduma za Jamii, Taasis inayofuata ni Taasis inayoongozwa na Viongozi hawa: Maaskofu, Mapadre, Watawa (Mabrother na Masista) yaani Kanisa Katoliki. Na usipolitaja Kanisa Katoliki kwa hilo utakuwa aidha haujui au unachuki binafsi.
9. Viongozi wa Kanisa Katoliki wanaupenda UKWELI. Na Mtumishi wa Mungu Father John Hardon, SJ aliwahi kusema, "Our Duty as Catholics is to know the Truth; to live the Truth; yo defend the Truth; to share the Truth with others; to suffer for the Truth" (Kazi yetu kama Wakatoliki ni kuujua Ukweli; kuuishi Ukweli; kuulinda Ukweli; kuutetea Ukweli; kuwashirikisha wengine Ukweli; kuteseka kwaajili ya Ukweli).
Na kimsingi huyo UKWELI ni YESU KRISTO. "Yesu akawaambia, 'Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba; ila kwa njia ya Mimi'" (Yohane 14:6)
10. Kutokana na ukweli huo, Viongozi hao wa Kanisa Katoliki huheshimiwa sana na Waamini wao. Na hapa nikuambie tu ukweli kwamba kwa Muamini Mkatoliki, anawaheshimu Viongozi hawa pengine kuliko Kiongozi wa aina yoyote ile unayoijua wewe.
Na linapotokea jambo lenye ukinzani kati ya Viongozi wao na Mtu au kundi fulani la watu, ni rahisi sana kwa Mkatoliki kuufuata upande wa Viongozi wao. Ukitaka kuamini hiki ninachokuambia, fuatilia suala zima la TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA (TEC) KUHUSU MKATABA WA BANDARI.
Sio kwamba Waamini hawa Wakatoliki wanafuata tu mkumbo la hasha. Hii ni kwasababu wanawajua vizuri sana Viongozi wao kuwa wako serious (makini) sana na mambo yao. Ni Viongozi ambao wanaongea wanachokimaanisha na wanakimaanisha wanachokiongea.
Sio kama walivyo baadhi ya Viongozi wengi wanaoleta Propaganda za kishamba na Siasa za kitoto ambazo zina athari kwa Jamii wanayoiongoza halafu wenyewe hawajali, wabinafsi na wanaoyajali matumbo yao tu bila kuwa na jicho la huruma kwa raia wengi wanaotaabika kwenye wimbi la ufukara ulipitiliza.
Viongozi ambao wakati mwingine unaweza ukadhani labda Akili zao zina makengeza. Wanatamani kukiona hiki ila macho hayana ushirikiano na mshikamano na uso wao. Ni Viongozi ambao wanajua Ukweli lakini hawako tayari kukusema ukweli au wanaogopa kumshauri Boss wao kisa tu Boss ameshaonesha mwelekeo fulani wanaoujua kwahiyo wanaogopa kumshauri tofauti na ukweli kwa kuogopa kuvipoteza Vyeo vyao.
Very hopeless Leaders!!
11. Viongozi wa Kanisa Katoliki wana BUSARA. Na ninaposema Busara namaanisha, "Matumizi sahihi ya Maarifa". Ni wasomi walioelimika. Yaani ni wasomi wanaojua kuitumia Elimu yao kwa manufaa yao na manufaa ya Jamii inayowazunguka.
Unajua, hapa Tanzania tuna Wasomi wengi sana na tuna Viongozi wengi sana Wasomi ambao hawajafanikiwa kuelimika. Waliosoma ni wengi ila walioelimika wako wachache sana. Wengi wamesoma ila wachache wameelimika.
Ndio maana tuna baadhi ya Viongozi ambao jinsi wanavyotumia Elimu na Akili zao katika baadhi ya Maamuzi huwezi kuamini kama kweli walifundishwa na Walimu wenye Vyeti halali au ni wale wa Vyeti Feki. Ukiwasikiliza jinsi wanavyotengeneza Logic zao katika maongezi unaweza ukadhani labda ni watoto wanaojifunza kuongea.
12. Viongozi wa Kanisa Katoliki ni mfano halisi wa MCHUNGAJI MWEMA ambaye Yesu Kristo Mwenyewe kwa kinywa chake alimsema, "Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema hutoa nafsi yake kwa ajili ya kondoo...... Mimi ndimi mchungaji mwema, nawajua walio wangu, nao walio wangu wanijua Mimi" (Yohane 10:11,14)
Mchungaji Mwema ana sifa kuu Tatu:
1. Mwema
2. Huitoa nafsi yake kwaajili ya kondoo wake
3. Huwajua kondoa wake nao walio wake wanamjua
Hawa Viongozi ni WEMA kwa kuwa wana NIA NJEMA na Wakatoliki na hata wale wasiokuwa Wakatoliki yaani ambao hawamo katika 'Zizi' la Ukatoliki (Yohane 10:16). Maana yake Mapadre na Maaskofu wetu ni WEMA kwa Watanzania wote.
Viongozi hawa WANAZITOA NAFSI ZAO kwaajili ya Taifa la Mungu. Ndio maana wanapambana kuzitetea Rasilimali za Taifa hili kwa manufaa ya Watanzania wote japo wasiojua wanawatukana badala ya kuzijibu Hoja zao kwa Hoja.
Wanawajua Waamini wao wanataka nini na Waamini wao nao wanawajua Viongozi wao na wanawaheshimu. Ndio maana nilisema kwa Mkatoliki kindakindaki, huwezi kumwambia chochote kinyume na Wachungaji wao akakuelewa. Hii ni kwasababu Maaskofu na Mapadre wanajuana na Waamini wao.
Hapa nimejaribu kugusia tu kwa uchache kuhusu namna Padre wa Kanisa Katoliki anavyopitia Maisha ya Kimalezi ya Kiroho, Kielimu na Kijamii kwa wale wenye Wito wa Upadre. Lakini kama ulikuwa umenifuatilia toka mwanzo nimeelezea kuhusu upatikanaji wa Viongozi hawa na Elimu zao. Sasa kazi ni kwako kupima kati ya Elimu ya Viongozi wa Kanisa Katoliki na Elimu ya hao Viongozi wanaokuongoza Kidini au Kisiasa nani wanatumia vizuri Elimu na Maarifa yao?
Niishie hapa!!