Suala la kumjua Mungu ni suala pana sana na linahitaji maarifa ya Ki-Mungu zaidi pia hili suala la kumjua Mungu ni suala la mtu binafsi kwasababu kila mmoja huhitaji kumjua Mungu kwa viwango tofauti tofauti na kwa namna tofauti tofauti

Pia ipo  tofauti kubwa sana ya ukimjua huyu Mungu na kunawengi wanamjua Mungu kama jina tu yaani kikawaida tu. Mfano mimi naweza nikawa namjua  Ambile; yaani namjua kwa jina tu ila sijui wadhifa wake sijui anakaa wapi anajishugulisha na nini ila namjua tu jina kuwa ni Ambile.

Hivyo hivyo kuna watu wengi hawamjui Mungu kiundani zaidi bali wanamjua jina tu kuwa ni Mungu sasa wewe ambaye humjui Mungu kiundani zaidi usitegemee kitu kutoka kwake kwasababu Bwana huwajua walio wake…

Wewe usiyemjua nayeye hakujui….

Mtu asiyemjua Mungu kiundani zaidi yupo sawa na wa mataifa kwasababu hata watu wa mataifa hili jina la Mungu wanalijua vizuri  tu ila shida hawazijui kazi zake na umuhimu wa jina lake ndio maana katika Mathayo alisema kuwa si kila mtu aniambiaye Bwana Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni.

Mathayo 7:21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

Alisema vile kwasababu kumwita au kumjua sio shida ila shida ipo kwenye utendaji.

Sasa leo wacha nikupe baadhi ya hizi mbinu au maarifa yatakayokuwezesha kumjua Mungu mimi sijui unataka kumjua Mungu kwa namna gani au kwa kiwango gani au kwa sababu gani wewe mwenyewe ndo unajua.

2a. MAANA YA MAARIFA:

Nini maana ya maarifa? Maarifa ni ujuzi au elimu juu ya kitu au juu ya jambo fulani.

2b. MUNGU NI NANI NA KWANINI TUMJUE?

MUNGU: Ni Mungu ambaye aliumba au muumbaji wa ulimwengu wote yaani yeye ndiye aliyevifanya vitu vyote vya hapa duniani na nje ya dunia, vile tunavyoviona na vile tusivyoviona yeye Mungu kavifanya vyote hivyo na bila yeye hivi vyote visingekuwepo hata sisi wanadamu tusingekuwepo ukisoma kitabu cha mwanzo sura ya kwanza Neno lipo wazi kabisa.

Wakolosai 1:16 Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.

KWANINI TUMJUE MUNGU?

Hapa sitaelezea sana jibu la hapa nitaelezea zaidi kwenye sifa za kumjua Mungu kiufupi ni hivi tunamjua Mungu kwasababu ndiye kimbilio letu kwasababu kwake kuna uzima wa milele

Yohana 17:3 Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.

3. NJIA ZITAKAZOKUWEZESHA KUYAPATA MAARIFA YA KUMJUA MUNGU:

I. Ni lazima uwe msomaji wa Neno la Mungu.

Neno la Mungu ndiyo dira yetu sisi wakristo Neno la Mungu ndilo linalotuwezesawa.kuyajua yoote yaliyoandikwa kwenye biblia bila Neno la Mungu basi hatuwezi kuelewa chochote.

Hebu tuone mfano wa wale mafarisayo walikuwa wakimhoji Yesu kwa habari ya kiama.

Marko 12: 20-24 Basi kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?

Walikuwa wanauliza vile kwasababu walikuwa hawasomi biblia walikuwa hawajui nini kimeandikwa kwenye biblia ndio maana Yesu aliwaambia wanapotea kwakuwa walikuwa hawayajui maandiko.

Hivyo ili uweze kumjua Mungu ni lazima uwe msomaji wa Neno lake kwa sababu Neno la Mungu ndo litakalokuongoza kwa kila kitu na si vinginevyo.

2 Timotheo 3: 16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; 17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

Neno linasema kila andiko lenye mpumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho.

Neno la Mungu hutukamilisha ili tuweze kutenda kila lililo jema sasa ukiwa husomi Neno la Mungu huwezi ukajua hili ni jema au baya kivyovyote kwako utaona ni sawa tu.

Wapendwa tusome Neno la Mungu ili tuweze kupata upeo na maarifa ya kutuwezesha kumjua Mungu kwa undani zaidi.

Kadiri utakavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo utakavyozidi kumjua huyu Mungu kwa undani na kwa uzuri.

Huwezi ukawa na maarifa ya ki- Mungu ikiwa kutwa mzima unashinda kwenye magroup ya kidunia kila kukicha wewe na facebook kila kukicha wewe na instagram mitandao yote wanakujua lakini hakuna hata cha maana unachoambulia bali ni umbeya tu na ukitoka huko mtandaoni wewe na remote kuangalia tamthilia yaani huna mda kabisa wa kusoma biblia, sasa kwa staili hiyo maarifa ya ki-Mungu utayapataje?

Neno la Mungu linasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa  nikweli kabisa tunaangwamizwa ni kwasababu  hatusomi Neno la Mungu  tunapenda miujiza ndio maana tunapotoshwa na mafundisho ya uongo  Kwa sababu ya kukosa maarifa ya Ki-Mungu na haya maarifa yanapatikana kwa Neno la Mungu tu na si vinginevyo labda kama unataka maarifa mengine sio ya Ki-Mungu hayo unaweza ukayapata hata huko kwa group za kidunia hata mitaani lakini Maarifa ya Ki-Mungu yanapatikana kwa Neno lake Mungu mengine ni kupotoshana tu.

Pia Neno linasema kila apendaye mafundisho hupenda maarifa sasa wewe usiyependa mafundisho toka kwenye Biblia hayo maarifa utayapata wapi?

Wapendwa tusiwe wavivu tusome Biblia kwa faida yetu wenyewe tenga mda wako wa kusoma biblia jiwekee mkakati wa kusoma biblia kwa siku hata vifungu viwili na kuendelea ndipo utaweza kupata haya maarifa ya kumjua Mungu vizur.

II. Weka kiu ndani yako ya kumtafuta Mungu kwa bidii.

Katika Mithali 8:17 Mungu anasema nawapenda wale wanipendao, na wale wanitaftao “kwa bidii” wataniona hajasema kwamba na wale wanitaftao akaishia hapo bali alizidi kusema na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

Sasa kumbe ili uweze kumjua Mungu ni lazima umtafute kwa bidii sana kwamoyo wako wote na kwa nguvu zako zote.

Mungu huwa ajishughulishi kabisa na wale wamtaftao kwa ulegevu na huwezi ukamjua Mungu ikiwa hujaweka bidii na kiu ndani yako ya kumtafta yeye.

Mpendwa kila kitu kinapatikana kwa juhudi na bidii sisi wenyewe ni shahidi kwa hili huwa tunafanya mambo yetu ya kimwili kwa bidii sana ili tufanikiwe.

Vinyo hivyo hata kutafta mambo yetu ya kiroho ni lazima kuwa na bidii …bidii yako ya kumtafta Mungu ndiyo itakufanya umjue Mungu kwa kina zaidi na kwa kiwango unachotaka wewe.

Kumbukumbu la Torati 4:29 Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.

Mtafte Bwana Mungu wako kwa bidii na kwa moyo wako wote Neno linasema ukimtafta kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote utampata

Yeremia 29:13-14 Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema Bwana, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka.

Ndugu yangu Neno linazidi kitusisitiza sana tutamjua au tutamuona ikiwa tunamtafta kwa moyo wote …hivyo mpendwa ninakusihi uweke kiu ndani yako ya kuweza kumjua Mungu zaidi na kimtafta kwa bidii.

Wafilipi 3:8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;

Mtume Paulo alikuwa na kiu kubwa sana ndani yake katika kumjua Mungu ndio maana mambo yote aliyaona si kitu kwake mambo yote alioni ni hasara bali alichokuwa akipigania ni kumjua Mungu.

III. Kuwa karibu na Mungu kwa maombi.

Njia hii pia itakuwezesha kumjua Mungu zaidi  jenga tabia ya kukaa faragha kwaajili ya kuzungumza na Mungu wako Yesu alikuwa akijitenga na wanafunzi wake anaenda mlimani kuomba peke yake hii ni kwa sababu ili uwe na wakati mzuri wa wewe kuwasiliana na Mungu wako kusiwe na kelele yeyote mawazo yako yote fikira zako zote  na moyo wako unauelekeza kwa Mungu.

Mathayo 14:23 Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.

Jizoeze kuomba kila wakati kadiri unavyozidi kuomba ndivyo na Mungu atazidi kujifunua kwako zaidi na ndipo utaweza kumjua zaidi na zaidi.

Tukisoma biblia tunaona Mungu alijifunua kwa Eliya kwa sababu ya kuomba Mungu alijifunua kwa Dauni kwa sababu ya kuomba na ukizidi sana kusoma biblia utaona njisi Mungu alivyojifunua kwa watumishi wake kupitia maombi; …hivyo nawe  kuwa karibu na Mungu kwa maombi hakika atajifunua kwako  na utamjua zaidi.

Zaburi 105:4 Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote.

IV. Unyenyekevu.

Unyenyekevu unahitajika sana kwenye suala la kumjua Mungu.

1 Petro 5:5-6 Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;

Mungu hupingana na wenye kiburi kwahiyo wewe uliye na kiu ya kuweza kumjua Mungu alafu umejaa kiburi ndani mwako nakwambia Mungu hatokuwa na habari na wewe kabisa kama ni kuomba utaomba sana lakini hotafanikiwa lolote kwasababu moyo wako umejaa kiburi na Mungu hapendezwi wa watu wa namna hiyo.

Hivyo kama unahaja ya kimjua Mungu basi jifunze kuwa na moyo wa unyenyekevu usiwe na moyo wa kujiinua.

Yesu anasema tujifunze kwake kwakuwa yeye ni mpole na mnyenyekevu hivyo basi Yesu anatutaka tufuate nyanyo zake.

Mathayo 11:29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

V. Kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.

Kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ni pamoja na kutii amri zake ni lazima uenende sawa sawa na mapenzi yake ni lazima kuishi maisha ya utakatifu na kuliamini jina lake.

1 Yohana 2:3-6 Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.

Isaya 57:15 Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.

Mungu wetu ni mtakatifu kwahiyo nawewe ili uweze kumjua ishi maisha matakatifu yenye kumpendeza yeye ni pamoja kuwa mtu kutubu kila wakati pale ukihisi ujaenda sawa sawa.

4. FAIDA ZA KUMJUA MUNGU:

A. Kupata WOKOVU na kuwa na UZIMA WA MILELE.

Yohana 17:1-3 Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.

Haya ni maneno ya Yesu Kristo anasema kuwa na uzima wa milele ndiyo huu wakujue wewe Mungu wa pekee wa kweli.

Sasa basi kumbe ukishamjua huyu Mungu wetu aliye hai unakuwa na uzima wa milele ndani mwako unakuwa na tumaini la kuingia Ufalme wa Mungu.

Matendo ya Mitume 4:12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.

Mwana wa Mungu asikudanganye mtu hakuna wokovu katika mwingine awaye yote wala hakuna jina jingine ambalo tumepewa wanadamu litupasalo kuokolewa bali ni wokovu wa Mungu pekee.

Na wokovu huu huja pale umapoamua kumjua na kumwamini huyu Mungu wetu wa mbinguni.

Mpendwa tamani leo kumjua huyu Mungu ili uwe na wokovu na upate uzima wa milele.

B. Ukimjua Mungu unakuwa na AMANI ndani mwako.

Ayubu 22:21 Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.

Neno linasema kuwa mjue sana Mungu ili uwe na amani ndivyo mema yatakavyokujilia.

Hapa tunapata vitu viwili pale tunapomjua huyu Mungu;

✔ Unakuwa na amani ndani yako na

✔ Mema yanakujilia

Ukimjua huyu Mungu yaani amani inatawala ndani mwako unaishi maisha ya amani kabisa unaishi bila wasi wasi wowote.

Unaenda kila mahali unapita kwa mfano kule kijijini kwetu kunamahali zipo njia watu hawapiti kabisa usiku huwa wanahofia kutekwa na kufanyiwa unyama fulani.

Lakini wewe Mungu unayemjua unajua kuwa yuko mahali pale umaweza pita tu wala hutodhuriwa na kitu kwasababu unajua Mungu wa miungu upo naye mahali pale basi utapita bila shaka kabisa.

Pia ukishamjua huyu Mungu mema yoote yanakujilia kwako Mungu atakuepusha na kila mambo yaliyo mabaya Mungu atakukinga dhidi ya adui zako mafanikio yatakujilia kwasababu mafanikio mazuri yapo mikononi mwake Mungu.

Ukisoma Mathayo 6:25-33 Neno linasema tuutafute kwanza ufalme wake Mungu na yale yoote ambayo tunahitaji atatuzidishia… ikiwa ni mafanikio ya kimwili au kiroho, Yeye ameahidi kuwa atatuzidishia kwasababu mafanikio yote yapo mikononi mwake.

Pia tutapokea baraka zote za rohoni na za mwilini na atafanyika mlinzi wetu.

C. Kiwango cha IMANI huongezeka.

Uzoefu wako wa kumjua Mungu utakufanya uzidi sana katika imani hatatokea mtu yeyote mwenye kukubabaisha kwa maneno hata hawa nabii wa kigeni wa (uongo) hawatakubabaisha kwa miujiza yao na kwa maneno yao ya uongo kwa maana kweli yote kuhusu Mungu utakuwa unaijua …pia uzoefu wako wa kumjua Mungu utakufanya uzidi sana kukua kiroho.

5. HITIMISHO:

Mtu wa Mungu tamani sana siku zote kimjua Mungu tamani kukaa uweponi mwake siku zote tamani kujifunza neno lake tamani kuyajua matendo yake makuu upendo wa Yesu uwe pamoja nawe tamani Yesu Kristo akae moyoni mwako.

Waefeso 3:17-20 Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;

Zaidi sana usiwe mwenye kujisifu kwa sababu unayo hekima usijisifu kwasababu ya nguvu zako usijisifu kwa utajiri ulionao zaidi ya hayo yote Mungu anasema bali ajisifuye ajisifu kwasababu hii ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua.

Yeremia 9:23 Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; 24 bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,

Sasa wewe unayejisifu kwa sababu ya vitu ulivyonavyo badala ya kujisifu kwasababu unamjua Mungu wakati huo vitu vyoote hivyo unavyojisifia ni mali yake Bwana je si zaidi sana kujisifu kwaajili yake?

Hebu soma na hii mistari…

1 Wakorintho 1:19-21 Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?  Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa.

Mwenyezi Mungu awakubariki sana!

Napenda kuwashukuruni nyoote mliokuwa pamoja nami kwenye kipindi hiki. Endelea kufuatilia semina hii kwa siku mbili zilizobaki ili uzidi kujifunza zaidi.