Friday, June 26, 2020

KUMTUMIKIA MUNGU NI NINI ?

KUMTUMIKIA MUNGU NI NINI?
Martin Luther King alisema"Fundi viatu mkristo hataweka misalaba midogo midogo kwenye kiatu anachotengeneza ili kuonyesha ukristo wake, bali atatengeneza viatu vizuri na imara".
Wengi tunajua kumtumikia Mungu ni nini...lkn leo nataka tuongeze ufahamu kidogo tu. Tujue zaidi.
Kumtumikia Mungu ni kufuata yale ambayo anatuagiza tuyafanye kwa kiwango kitakacho mfanya yeye Mungu kuwa Mkuu sana. Ni kujikabidhi kwake na kufanya yale yampendezayo kwa namna ambayo utukufu wake utaonekana.
Joshua 24:15
Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.
Kumtumikia Mungu ni neno pana sana. Ni zaidi ya kushinda kanisani. Ni zaidi ya kusafisha kanisa. Ni zaidi ya kujenga kanisa kuuubwa. Ni zaidi ya kuimba praise team na kwaya. Ni zaidi ya kutoa sadaka nene. Ni zaidi ya kuwa mzee wa kanisa na mhubiri. Kumtumikia Mungu ni kule kuishi kwa unyoofu ambao tunakuwa kielelezo kwa wengine na hivyo utukufu kurudi kwa Mungu.
Matendo ya Mitume 17:24-25
Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu. 25 Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na anawapa kila kitu.
Kumtumikia Mungu ni tofauti na kutumikia wanadamu. Wanadamu hupokea kitu kutoka kwako pale unapowatumikia la sivyo kuna madhara yatatokea. Mungu hata kama anasema anataka sifa, asipopokea hapati madhara yoyote. Ataendelea kuwa Mungu na ukuu wake unabaki palepale. Anachotaka kwetu ni uchaji tu. Tena ni kwa ajili yetu zaidi.
Mzee Petro anaandika maneno magumu kidogo kuhusu utumishi. Msikie..
1 Petro 4:11
Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumika anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.
Huo ndio utumishi. Kuna mahali Yesu anasema "msiposifu ninyi mawe yatasifu". Ana maanisha, kama wasipofanya wale waamini,basi hata wasio waamini watafanya. Mungu atamtumia hata asiyemjua yeye Mungu kutimiza kusudi lake. Kumbuka,kusudi la Bwana husimama hata iweje. Iwe mvua au jua. Mawio au machweo.
Ukimcha Mungu, vitu vitakutumikia. Usiseme sina chochote, wewe si mahiti. Tumika kwa kidogo ulichonacho maana Mungu wetu yeye huangalia moyo.
Kuna mtu alimuomba Yesu ruhusa ya kwenda kuzika mzazi wake, lakini pamoja na heshima ya mahiti, Yesu akamwambia waacheni wafu wazike wafu wao. Yesu hapa alikuwa akionyesha uthamani wa kumtumikia Mungu haulinganishwi na kitu chochote.
Muinjilisti Marko ananukuu Maneno ya Yesu juu ya utumishi
Marko10:45 "Maana hata mimi Mwana wa Adamu sikuja ili nitumikiwe, bali nilikuja ili niwe mtumishi na kutoa maisha yangu yawe fidia kwa ajili ya watu wengi.”
Kujitoa kwa ajili ya wengine ndio utumishi. Wale ambao hawapo kwa ajili ya kutumikiwa bali kutumika ndio watumishi. Na sio other way around. Lkn watumishi wa leo wengi wetu hatupendi kutumika tu. Tunapenda kutumikiwa na kama sio kutumikiwa basi tupate kitu kutoka kwa hao tunaowatumikia in return!
Warumi 12:1-2
Kwa hiyo ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, jitoeni kwake muwe sadaka hai, takatifu na inayompendeza Mungu, ambayo ndio ibada yenu ya kiroho. 2 Msiige tabia na mienendo ya dunia hii bali mbadilishwe, nia zenu zikifanywa kuwa mpya, ili mpate kuwa na hakika ni nini mapenzi ya Mungu: yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na makamilifu.
Paulo anatuambia kuwa kwakuwa tumepata wokovu kwa damu ya Yesu,sasa ni jukumu letu kujitoa sisi wenyewe kama sadaka hai mbele za Mungu (kama shukrani zetu kwa Mungu au sadaka kwa Mungu) huku tukichukua tabia mpya za nje ya dunia hii (mbinguni). Kwa kufanya hivyo tutaweza kuyajua mapenzi ya Mungu kwetu ili tuishi kwa ukamilifu na kumpendeza yeye ambako ndiko kumtumikia Mungu.
Petro anasema( kwenye hiyo 4:11) kuwa,kila mtu atumie kipawa alichopewa kwa uaminifu. Popote pale ulipo kazi yako na yangu ni kuwa balozi wa Mungu kupitia matendo yetu katika mahali tulipo. Kila MTU atumie kipawa chake kwa namna ambayo inamuinua Mungu. Ndio maana ya kuwa kielelezo. Pale watu wengine wanapotutazama kwenye mambo yetu na kila kitu tunachofanya kama wakristo wamuone Mungu. Wauone Upendo wa Mungu. Wauone uwepo wa Mungu.
Martin Luther anasema yule fundi viatu anapoweka misalaba midogo midogo kwenye kiatu FEKI,hapo hajawa mkristo wa kweli kwa kuweka hiyo misalaba. Kwanini? Hajatumia talanta au kipaji chake kwa uaminifu. Kumbe UAMINIFU ndio msingi wa utumishi.
Vipawa tulivyonavyo ni kwa ajili ya kumpa Mungu utukufu na kuwasaida wengine. Nia ya Mungu kwenye hii dunia ni kufanya kuwa mahali pazuri sana pa kuishi. Na nia hii inatimia kupitia sisi ambao ndio tunakaa kwenye hii dunia. Hakuna mtu asiye na kipaji chochote. Kila mtu ana kipaji labda kama hajui kipaji chake. Sasa vipaji ni vya nini? Kwanini wanadamu tupewe vipaji ndani yetu? Ni kwa ajili ya kuwatumikia wengine na utukufu urudi kwa Mungu.
Leo wengi tunadhani kumtumikia Mungu ni kusimama madhabahuni na kuhubiri. Au kuwa wazee wa kanisa. Au kuimba kwaya flani au kufanya chochote ndani ya kuta za kanisa. Lkn si wote wanaweza kupata nafasi za kufanya hayo. Wengi hujikuta wana maisha nje kabisa na mbali ya kanisa. Kumbe hapo ulipo ndio utumishi wako ulipo.
Twaweza kumtumikia Mungu kwa..
1)Kusambaza Upendo.
Wagalatia 5:14
"Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”
Inashangaza ambavyo tunaishi pamoja lkn hatujishughulishi kujuana. Tunawekeana mipaka ambayo haina upendo ndani yake. Kwa mfano ,mlinzi wa geti Ia kanisa lako,umeshawahi kumuuliza mara ngapi familia yake inaendeleaje wakati unampa kadi ya kukuruhusu kutoka na gari yako? Shoe shiner(muosha viatu) wa pale ofisini kwenu je? Yule mpika chai wa ofisi? Anayekuoshea gari je? Unadhani wao wanakutazamaje? Lini umeshawahi kuwa" tip"kama unavyowatip kule kwingine? Kupeana moyo,kuongea kwa Upendo ndio kutumika huko. Tunakuwa mfano wa maisha ya ukristo kweli.
2)Kuwasaidia wenye uhitaji
Mathayo 25:40
“Mfalme atajibu, ‘Ninawaambia kweli, kwa jinsi ambavyo mlivyomfanyia mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinifanyia mimi.’
Kuna mambo madogo madogo mengi ambayo hatuyapi umuhimu kwetu lkn kwa Mungu yana maana sana. Unaweza ukainunulia familia flani masikini unga kidogo na kuwapatia kwa ajili ya chakula chao cha mlo mmoja. Machoni kwa Mungu hicho ni kitu kikubwa sana. Mungu kawaumba hao kuleta uwiano baina yetu. Au kumsaidia bibi kuvuka barabara.. Kumpisha mama mjamzito au mzee kwenye seat ya daladala ni vitu vidogo lkn vina maana kubwa. Kadri tunavyowatendea hao ndivyo tunavyomtendea Mungu. Sio lazima uende Orphanage Centers na makamera kedekede ili kuwatangazia watu unayofanya. Haufanyi kwa wanadamu bali kwa Mungu.
Waebrania 13:2
Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua.
3) Kuitafuta hekima
Mithali 16:16
"Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha".
Visu hunolewa. Magari huitaji mafuta na mkristo anahitaji hekima ya Mungu na ufahamu. Ni jukumu la kila mkristo kujibidisha kupata elimu juu ya Mungu. Maarifa juu ya Mungu. Sio vema kuacha kila kitu kwenye mikono ya wachungaji pekee bila sisi wenyewe kujibidisha kutafuta maarifa juu ya Mungu. Namna hii tunakuwa tunayajua mapenzi ya Mungu na hivyo kumtumikia. Kumbuka, kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe siku ile ya hukumu.
4)Samehe
Marko 11:24-25
Mnaposimama kusali, sameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. 26 Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.
5) Weka nafasi kwaajili ya ibada
(Wagalatia 5:24-25)
Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
Unapoamka asubuhi na kujiona mzima au unaumwa,unamshukuru Mungu? Unamtukuza Mungu? Kila ambacho anakifanya kwako na ukajiona upo hai bado ni cha kumshukuru yeye. Mwambie asante kwa kazi yako uliyonayo. Uhai wako. Ndugu zako. Kila kitu mshukuru maana kuna wengi hawana hivyo ulivyonavyo. Shukrani ni utukufu kwa Mungu.
Kumtumikia Mungu ni muhimu kwakuwa tunatimiza yale ambayo Mungu ametuumbia kuwepo hapa duniani na kuyafanya. Kila mtu pale alipo kwenye anachofanya akifanye kwa uaminifu. Akifanye sio kwa sifa binafsi bali kwa ajili ya kuwa kielelezo cha ukristo wake. Yani Kristo ainuliwe kupitia matendo yetu. Kila tunachofanya kifanyike kwa namna Mungu anayopenda tufanye. Ukiwa rubani, muosha magari, fundi muwashi, engineer, mfanyabiashara,mhasibu, nesi au popote pale ulipo kwenye hicho unachofanya, kifanye kwa uaminifu. Kwa kadri kilivyopaswa kufanyika ndio kumtumikia Mungu. Kuacha zile 10% ambazo si za halali. Rushwa. Kuonea wengine. Kuwachukia wengine, kuwasingizia wengine na mengine mabaya tuyajuayo hakumpi Mungu utukufu.
Kumbe unaweza ukamtumikia Mungu ukiwa mwanasheria, muhasibu, mkulima, mfugaji, mwalimu au yeyote pale ulipo,kitu kikubwa ni kufanya hicho ufanyacho kwa namna ambayo inamuinua na kumrudishia Mungu utukufu. Yani kila anayekuja kwenye nafasi yako anaona unyoofu.
Ndio mama Martin Luther King anasema,mkristo wa kweli hataweka misalaba kwenye kiatu anachotengeneza ili kuonyesha ukristo wake,bali atatengeneza kiatu madhubuti kuonyesha ukristo wake.
UELEWA ZAIDI KUHUSU KUMTUMIKIA MUNGU
Luka 13:22 - Mtu mmoja akamuuliza Bwana Yesu Je! Watu wanaookolewa ni wachache? Bwana akamjibu akamwambia jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawambia kuwa wengi watataka kuingia wasiweze.
Mahali pengine maandiko yanasema tangu enzi za Yohana mbatizaji habari njema ya ufalme inahubiriwa, na wenye nguvu wauteka huo ufalme.
KUMTUMIKIA MUNGU
Katika Mathayo 19:27 tunaona maneno ambayo mtume Petro alimuuliza Bwana Yesu kuwa walikuwa wameacha vitu vyote na kumfuata Yesu, Je! Watapata NINI? Mara nyingi napenda kusema kuwa hakuna mtu yeyote duniani mwenye akili timamu anayependa HASARA. Petro alitaka kujua atakachokipata, baada ya kuwa ameamua kuacha vyote na kumfuata Yesu. Kama ingetokea Bwana Yesu amjibu kuwa fanya kazi maana UNAJITOLEA, nadhani hapo ndipo ingekuwa mwisho wa Petro. Lakini kwa kumjibu alimwambia atapata mara mia, katika ulimwengu huu na uzima wa milele baadaye.
Habari hii pia tunaiona katika Marko 10:28-31 huku tofauti ikiwa ni kuongezwa maneno PAMOJA NA DHIKI katika Marko. Ndiyo maana katika Galatia 6:9 mtume Paulo aliandika maneno fulani ili kuwaambia Wakristo waendelee kufanya kazi ya Mungu bila kuchoka, maana malipo yapo baada ya kazi hii katika dunia hii. Maneno hayo ni:
Tena tusichoke katika kutenda mema, kwa maana tutavuna kwa wakati wake tusipozimia roho.
1Kor 15:58; “Basi,ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa mwajua kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana”. Yaani kazi ambayo italipwa ni ile iliyofanywa katika Bwana,( sio kazi yoyote, katika Bwana. Ndiyo maana anasema ni wale tu wafanyao MAPENZI YA BABA YANGU). Kumbe unaweza ukafanya kazi ya Mungu, lakini yakawa siyo mapenzi ya Mungu.
Katika Ebrania 6:10 tunaona kuwa Mungu si dhalimu hata aisahau kazi ya mtu. Hii ina maana kuwa Mungu hawezi kudhulumu mtu yeyote. Ndio maana imeandikwa “kila mtuatavuna kile alichokipanda”.
Faida ya Kumtumikia Mungu.
Faida utakazozipata kama ukiamua kumtumikia Mungu kwa dhati. Faida hizi ni zile utakazopata ukiwapo hapa hapa duniani. Najua tutalipwa pia na mbinguni, lakini leo naongelea faida za hapa hapa duniani.
-Mithali 11:31 – Mwenye haki atalipwa duniani, na mkosaji pia.
-Mithali 11:25 – Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa. Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe. Maana yake ni chochote unachofanya kwa watu, ujue na watu pia watakufanyia. Ukifanya ubaya, ndivyo utafanyiwa; Ukifanya wema ndivyo utafanyiwa.
-Mith 12:14 – Utavuna chochote utakachokipanda
.
-Mith 20:7 – Chochote utakachokifanya, kizuri au kibaya, utawaachia watoto wako. Wakati mwingine unaweza kudhani uko salama, kumbe utawaachia watoto wako ama BARAKA, au LAANA. Ukiangalia kwa makini katika 1Falme 4:24-25 kuna maandiko maneno yanayosema kuwa Sulemani alistarehe pande zote. Swali ni kwa ninialistarehe? Hii ni kwa sababu baba yake alikuwa amepigana vita vya kutosha, alikuwa amesukumia mbali maadui kiasi cha kuwa mbali sana na Ufalme wake Sulemani.
-Mith 13:22 – Huwaachia WANA WA WANA–
Unaona sasa imekwenda kwa WAJUKUU. Ndiyo maana tunasema Mungu wa IBRAHIM, ISAKA, na YAKOBO. Leo hii watu wengi wanahangaika kwa sababu ya yale ambayo baba, babu zao walifanya; Wao wanahangaika leo, au wanafurahia leo.
-Luka 7:2-5 -Kuna maneno yanayoonyesha jinsi Wazee walivyomwambia Yesu kumtendea jambo jema mtu ambaye aliwajengea sinagogi. Hivyo kwa kuwa alijenga SINAGOGI basi alistahili kutendewa jambo hilo. Kumbukumbu ni muhimu sana. Leo hii kuna watu wameshapita lakini hakuna kumbukumbu lolote. Walikuwa na mali, walikuwa na uwezo, lakini leo hakuna kumbukumbu lolote kuwa walikuwepo duniani.
-Mith 10:27-Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu. Mpendwa Neno linasema wazi wazi kuwa kama utakuwa ni mcha Mungu miaka yako itaongezwa, mahali pengine inasema AKASHIBA SIKU.
Katika Isaya 54:12-17 tunaona faida tupu kama ukimcha Mungu, sitaikopi hapa, tafadhali tafuta muda uisome uone. Waweza soma pia faida tele katika Isaya 43:2 na uone kuwa hakuna hasara yoyote katika kumcha Mungu.
-Ayub 5:19-27. Ayubu alikuwa ni mzee wa siku nyingi hivyo alijua faida tele za kumtumikia Mungu. Ndiyo maana aliandika namna hiyo hapo, ebu soma uone!
Watu waliomtumikia Mungu na kuona faida zake, ambao habari zao tunazipata katika Biblia. Pata muda usome maandiko kuhusu mifano hii:
-Mdo 9:36-Dorkas.
-Isaya 38:1-Hezekiah.
-Esta 3:12-Mordekai.
-Mdo 10:1-Cornelio